Saturday, 28 June 2014 03:00

Ada vyuo vya ualimu zazidishwa

Na Mwandishi wetu.
Serikali imepandisha maradufu ada kwa wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vya ualimu nchini kuanzia muhula ujao wa masomo.
Ada hizo kwa wale wa ngazi za cheti na stashahada ambazo zimeongezwa kwa karibu mara mbili au zaidi ya zile zilizokuwa zikilipwa awali. Uamuzi huo ambao huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi ambao waliona ualimu kama kimbilio, unaelezwa na baadhi ya wadau wakiwamo walimu, wanafunzi na hata wakufunzi wa baadhi ya vyuo nchini kuwa ni wa ghafla.


Kwa mujibu wa baadhi ya wakufunzi, uamuzi huo umetolewa kupitia waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na unatarajiwa kuanza kutekelezwa muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai 2, mwaka huu.
Kabla ya kupandishwa kwa ada hizo, wanafunzi wanaosomea ualimu kwa ngazi ya cheti walikuwa wakilipa Sh200,000, lakini sasa watalazimika kulipa Sh300,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.


Kwa wale wanaochukua stashahada watalazimika kulipa Sh400,000 kwa masomo ya Sanaa na Sh600,000 kwa masomo ya Sayansi kutoka Sh200, 000 za awali.


Mhasibu wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara, aliyekataa kutaja jina lake kwa kuwa siyo msemaji wa chuo hicho, alithibitisha kupokea waraka wa Serikali unaowataka kupandisha ada, lakini alisisitiza kuwa Mkuu wa Chuo ndiye angeweza kufafanua zaidi kuhusu ongezeko hilo.
“Taarifa hizo ni za kweli ada imepanda, kama umezipata kutoka wizarani hivyo ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu ya kupata taarifa zaidi kutoka kwetu,” alisema mhasibu huyo.


Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na uhaba wa fedha na ugumu wa kuviendesha vyuo hivyo.
Habari zinasema kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikidaiwa na wazabuni fedha nyingi, jambo ambalo limeathiri pia uendeshaji wa vyuo vikiwamo vya ualimu.


Baadhi ya wakufunzi wameeleza kuwa fedha za ada sehemu yake itatumika kutatua matatizo ya uhaba wa fedha ambao umekuwa ukiwakabili na hivyo kuathiri utoaji wa huduma zikiwamo za vyakula.


Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema viwango vilivyoongezwa siyo vikubwa ikilinganishwa na hali ya ugumu wa maisha ilivyo sasa nchini.

Read 2828 times