Thursday, 22 May 2014 03:00

Barabara 41 kujengwa kiwango cha lami

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli

Na Mwandishi wetu.
Wizara ya Ujenzi imepanga kujenga barabara 41 na madaraja 13 nchini kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 3,074, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Dar es Salaam-Chalinze yenye urefu wa kilomita 100 kwa mwaka 2014/15.

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15, alisema ujenzi wa barabara na madaraka hayo utagharamiwa na serikali na wahisani.

Alisema barabara ya Dar es Salaam-Chalinze- Morogoro (km 200) kwa kiwango cha 'Expressway' utagharimu Sh. milioni 750 na kwamba maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo yanaendelea na utatekelezwa baina ya serikali na sekta binafsi.

Dk. Magufuli alisema awamu ya kwanza itakuwa kilomita 100 kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na kiasi cha Shilingi milioni 100 zimetegwa.

Alisema barabara nyingine ni Wazo hill-Bagamoyo itakayogharimu shilingi milioni 10,885.24 ikiwa ni pamoja na kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ya Bagamoyo-Makofia-Msata kilomita 64 na ujenzi wa daraja la Ruvu Chini.

Barabara nyingine ni Usagara-Geita-Kyamyorwa kilomita 422, kigoma -Kigahwe-Upinzani-Kaliua -Tabora, Marangu -Tarakea-Kimwanga-Bomong’ombe- Sanya Juu yenye urefu wa kilomita 173, Arusha -Moshi-Holili kilomita 140, lengo ni kuchochea ukuaji wa Utalii katika  Mlima Kilimanjaro.

Nyingine ni Same -Himo –Marangu- Rombo -Lushoto kilomita 132, Kia-Mererani kilomita 26, Kwa  Sadala Machame-Masama-Machame kilomita 15.5 na Kiboroloni Kiharara-Tsudini-Kidia kilomita 10.80 zote zikigharimu Sh. milioni 13.133.63.

Barabara ya Nangurukuru-Mbwemkulu kilomita 95, Dodoma - Manyoni Kilomita 127, Mbwemkuru-Mingoyo kilomita 95, Dumila - Kilosa kilomita 78, Sumbawanga -Matai- Kasanga kilomita 112.

Nyingine ni Kayka-Bugene-Kasulu kilomita 178, Isaka-Lusahunga kilomita 242 na Lusahunga-Rusumo na Nyakasanza -Kobera kilomita 150, Manyoni-Itigi -Tabora na Korogwe -Handeni.

Madaraja yatakayojegwa ni ya Kirumi, Nangoo, Sibiti, Maligisu, Kilombero, Kavuu, Mbutu, Rehekei, Ruhuhu, Mombo, Simiyu, Wami na Lukuledi II. Hata hivyo, urefu wake haukutajwa.

Alisema baadhi ya barabara ilishaanza ujenzi na nyingine ndiyo zitaanza huku madaraja yakiwa katika hatua mbalimbali ya ujenzi na mengine yakihitaji upanuzi.

Barabara za mikoa zitakazokarabatiwa ni za  kilomita 685 za changarawe na za lami kilomita 78.

Read 2530 times