Monday, 09 April 2018 15:50

Mambo ya Kuzingatia Ndani ya Chumba Cha Usaili wa Kazi

Written by
Rate this item
(0 votes)

 

Usaili wa kazi ni moja ya mambo ambayo huleta msongo wa mawazo kwa watu wengi. Hofu kubwa uwa ni ya kushindwa kufanya vyema katika usaili. Kwa wale ambao hujiandaa vyema kwa kuzingatia mambo tuliyoelezana kwenye Makala iliyopita wao hofu upungua kwani siri ya mafanikio katika jambo lolote ni maandalizi mazuri.

JE, NI VIGEZO GANI HUANGALIWA KATIKA USAILI?

Kama haufahamu ni nini waajiri wanakitafuta kutoka kwako ili waridhike na waamue kukuajiri ni ngumu sana kufanya vizuri. Utakuwa kama mtu ajibuye maswali lakini hajui maswali hayo yanalenga kupima nini kutoka kwake.

Mambo mengi huangaliwa katika kupima uwezo wa mtu katika usaili lakini kati hayo mambo makubwa ni pamoja na ujuzi wa kuwasiliana. Katika hili waajiri juangalia namna unavyowasiliana nao katika kujibu maswali hasa unavyo ongea na kuhusianisha maongezi yako na viongo vya mwili wako kama mikono, macho, sura na mwili kwa ujumla. Suala jingine ni ujuzi na maarifa; katika hili waajiri hupima kwa kuuliza maswali ya kiweledi ya husuyo fani fulani mahususi au maswali ya jumla. Kama wewe ni Mhasibu wangependa kujua vitu unavyo vifahamu kuhusu kazi hiyo.

Katika mazingira mengine mtafuta ajira hutakiwa kuonesha ujuzi huo kwa vitendo na siyo kujibu maswali pekee. Kama ni kazi ya uwalimu unaweza pewa vifaa ufundishe. Kitu kingine ni kujiamini; jambo hili hupimwa kwa kuangalia jinsi unavyowasiliana na kuona kama una woga au wasiwasi. Sauti na sura yako vyaweza onesha dhahiri kuwa haujiamini.

Mambo mengine ambayo huangaliwa ni pamoja na ubunifu, ufahamu wa taarifa kuhusu taasisi unayotaka kufanyia kazi na mambo mengine ya ziada ambayo unayo. Katika mambo ya ziada tunazungumzia ni nini hasa ulicho nacho ambacho wengine hawana na taasisi itajivunia kuwa nawe kupitia hicho kitu.

Je, ni nini uzingatie unapoingia kwenye chumba cha usaili?

MATUMIZI YA MWILI KATIKA KUWASILIANA
Unapoongea hakikisha mwili wako unawiana na maneno yanayotoka mdomoni. Hii si siri kubwa sana katika kuwasiliana. Ukisema ninayo furaha kuwepo hapa hakikisha sura yako haipingi unachokisema-tabasamu. Vidole, mikono, macho na sura yako ishirikiane katika mazungumzo yako lakini hakikisha hauzidishi.

MTAZAME USONI ALIYE ULIZA SWALI
Chumba cha usaili kinaweza kuwa na watu kadhaa na kila mtu akawa na maswali yake. Kama mtu anauliza swali onesha umakini kwa kumuangalia na wakati unajibu fanya hivyo hivyo. Hii itaonesha ujuzi uliona katika kupeleka taarifa kwa mlengwa na kuwasiliana kwa ujumla.

KUWA MUWAZI KWA USICHOJUA
Hakuna mtu anayejua kila kitu. Hata anayekuuliza kuna vitu havifahamu kabisa lakini wewe unavijua vyema. Hii iwe sababu ya kuto kubabaika kama utaulizwa swali usilo lijua. “Nashukuru kwa swali, lakini ukweli ni kwamba sifahamu au sina taarifa kuhusu jambo hilo” kwa kujibu hivi inatosha kuwaonesha kuwa wewe ni mwaminifu na siyo muongo. Wapo watu ambao hujifanya wajuaji na hivyo kujibu kiholela. Hebu fikiria unaulizwa “Christian Ronaldo ni Rais wa nchi gani?” halafu unaropoka kwa sauti ya kujiamini “Chile”. Huwezi kujua kila kitu lakini jitahidi kujua vingi.

UNAPOKOSEA USIBABAIKE
Wakati mwingine unaweza jikuta umekosea kujibu swali kwa bahati mbaya, kwa kuchanganya taarifa au kukosea katika matamshi. Una nafasi ya kuomba kurudia ili kuweka kumbukumbu zako sawa au kurudia vyema neno ulilokosea. Endapo watakucheka wala usiwe na wasi wasi na wewe cheka kidogo. Stori itabadilika siyo watakuwa wanakucheka wewe lakini nyote kwa pamoja mtakuwa mnalicheka kosa ulilolifanya. Kujiamini ni muhimu sana.

OANISHA MAJIBU YAKO NA MAHITAJI YA KAZI
Kwa sababu usaili ni usaili wa kazi ni vyema kuhakikisha kuwa majibu yako yanahusiana na kazi yenyewe. Kwa mfano, ukiiulizwa ni jambo gani ambalo hautakuja kusahau maishani? Tafuta kisa ambacho kitaonesha kuwa ulitumia ujuzi wako kutatua tatizo au kilikuongezea ubora zaidi ambao ni muhimu katika ajira utakayopewa. Katika kila swali toa majibu yatakayo onesha wewe ni mbunifu, mvumilivu, mchapakazi, mkweli, mpenda watu, au sifa nyingine.

THIBITISHA KUWA KAZI INAKUHITAJI WEWE ZAIDI YA UNAVYOIHITAJI
Kwa kutokujua wapo watu wanaenda kwenye usaili kuthibitisha kuwa wanahitaji ajira. Huu ni ukweli ndiyo lakini usiegemee huko bali lenga kuonesha kuwa hiyo kazi ikikupata basi taasisi itakuwa imepata mtu sahihi. Usiseme eti nmeomba hii kazi kwa sababu sina ajira au kazi ninayofanya sasa hivi hainipi amani. Maelezo haya yataonesha unajifikiria wewe lakini taasisi inatafuta watu wanaoifikiria taasisi.

KUMBUKA KUTOA MIFANO
Moja ya vitu vianyowatofautisha watainiwa kwenye usaili ni uwezo wa kutoa mifano kwa yale wanayo yasema. Unaposema wewe ni mbunifu unaweza kutupa walau mfano mmoja wa kuthibitisha? Alikadharika unapozungumzia masuala kama kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na mengineyo. Mifano hii inatakiwa iandaliwe kabla hata haujaingia kwenye chumba cha usaili.

USIONESHE MISIMAMO ITAKAYOCHANGIA UBAGULIWE
Kila mtu ana machaguo yake na vitu anavyopenda na kuvisimamia. Dini, dhehebu, chama cha siasa, timu ya mpira na mengine mengi huonesha ni mambo gani tunayo yasimamia na kuyapenda. Lakini mambo haya yanaweza kusababisha tukabaguliwa. Ujapojibu maswali jiepushe na kuonesha misimamo ya kisiasa, kiimani na mengine kama haya.

Mwisho, kumbuka kufika mapema sehemu ya usaili na kuwa mtu mwema kwa kila unayekutana naye huwezi jua yeye ni nani kwenye taasisi au usaili huo. Wiki ijayo tutaangalia maswali ambayo huulizwa kwenye usaili mara kwa kwa mara na namna ya kuyajibu.

Read 420 times