Monday, 30 November -0001 02:27

Vyeti vyasitisha ajira 70 za watumishi KCMC

KCMC1.jpg

Moshi. Siku ya jana ilikuwa mbaya kwa kada tano za watumishi wapatao 70 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi, baada ya ajira zao
kusitishwa hadi wawasilishe vyeti vya kidato cha nne.

Habari za uhakika zilizopatikana na kuthibitishwa na uongozi wa hospitali hiyo inayomilikiwa na Shirika la Msamaria Mwema (GSF),
zilisema kadhia hiyo imewakumba watumishi wa Serikali tu.

Kwa mujibu wa waraka wa Utumishi wa Umma namba moja wa mwaka 2004, watumishi wote walioajiriwa baada ya Mei 20 mwaka huo na kuendelea,
walitakiwa kuwa na sifa ya kufaulu mtihani wa kidato cha nne.

Hata hivyo, waraka huo unaelekeza kuwa watumishi wa umma walioajiriwa kabla ya Mei 20, 2004 hawatalazimika kuwa na sifa ya kidato cha nne na
wataendelea na ajira zao katika utumishi wa umma.

Ingawa hospitali hiyo inamilikiwa na GSF shirika ambalo ni la kidini chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Serikali
inagharamia mishahara kwa watumishi wanaofanya kazi hapo wakitokea serikalini.

Fununu za kutekelezwa kwa waraka wa Serikali wa kuwaondoa kazini watumishi hao, zilianza kuzagaa juzi usiku baada ya kumalizika kwa kikao
cha menejimenti ya hospitali hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk Giliad Masenga alilithibitishia gazeti hili kuchukuliwa kwa hatua hiyo akisema ni
utekelezaji wa waraka wa Serikali kuhusu watumishi wenye elimu ya darasa la saba.

Kwa mujibu wa Dk Masenga, kada za wafanyakazi zilizoguswa na utekelezaji wa waraka huo wa Serikali ni pamoja na madereva, walinzi, wapishi,
wauguzi na wahudumu wa ofisi hospitalini hapo.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) mkoani Kilimanjaro, Emanuel Msuya alisema Tughe inazo taarifa hizo na
inachofahamu ni kuwa wamesitishiwa mishahara. “Hawajaachishwa kazi kama inavyozungumzwa mitaani, bali wamesitishiwa mishahara hadi watakapoleta
vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kumbuka walipewa muda mrefu wa kujiendeleza,” alisema.

Julai 13, 2017, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ilitoa taarifa kwa umma ikielekeza ambao hawajawasilisha
vyeti vya kidato cha nne wasitishiwe mishahara.

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Published in HABARI